SHERIA na sera
za dawa za kulevya bado hazijasaidia vita ya kutokomeza matumizi ya dawa za
kulevya Duniani kote; hivyo watungaji hawanabudi kuzipitia upya ili zisadie
wanaokumbwa na janga la matumizi ya dawa za kulevya
.
Hayo yalisemwa
na mwezeshaji na mwelimishaji wa vijana walioathiriwa na dawa za kulevya,
Damali Lucas, kutoka taasisi ya Medecine Du Monde (MDM), kituo
kinachojishughulisha na kuwasaidia vijana walioamua kuacha matumizi ofisini
kwake jijini Dar Es Salaam.
Alisema, sheria
na sera zilizoko zinamwathiri mtumiaji na siyo muingizaji na msambazaji; kwa
kuwa mara zote mtumiaji kwa jinsi kemikali hizo zinavyomfanya mwonekano wake wa
nje wa kutokujipenda kwa kuwa mchafu kila wakati, hivyo mara zote anaonekana
kuwa ni mhalifu.
Alisema kwa
kiasi kikubwa wamepata kesi za waathiriwa wa kemikali hizo haramu wamefikishwa
kituoni hapo wakiwa wamepigwa na kuumizwa vibaya na wananchi kwa kuonekana kuwa
ni wahuni na wahalifu; na pengine walipotaka kupata huduma katika hospitali au
vituo vya afya wameshindwa kupata haki zao za msingi kutokana na hali zao na
jamii kutokujua sheria inayowalinda.
Aidha, alisema
kuwa watunga sera wanatakiwa kuja na sera na sheria zinawasaidia kuliko kuwaona
kama wahalifu tu, wakati kuna kundi jingine ambalo linahusika na uingizaji
sheria haifanyi lolote kuwatia hatiani.
Hayo pia
yalithibitishwa na kijana, Mbwana Divai, Mkazi wa Dar Es Salaam, mtumiaji
aliyeacha na kuwa mwelimishaji wa vijana wenzake wanaotaka kuacha matumizi ya
kemikali haramu hizo; alisema kuwa kutokuwa na sera na sheria madhubuti
kumechangia kwa sehemu kubwa waathiriwa kukosa haki zao za msingi kama
kusikilizwa wanapougua na kwenda Hospitali; pamoja na kuwa wako katika matumizi
ya dawa hizo haramu.
Divai, alisema
yeye alianza kwa kuvuta sigara kwa muda na kuingia katika matumizi ya bangi
kutokana na makundi aliyokuwa nayo baada ya kufiwa na wazazi wake wote wawili;
ambapo alijikuta akijiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya, hivyo kusema
kuwa:
“Tumeshapata
matatizo katika jamii ya kutokuaminika hata kama unawaambia kuwa sasa umeacha
kutumia kemikali hizo, lakini bado imani inakuwa ndogo; ila kubwa zaidi sheria
na sera bado haziko vizuri kuweza kumsaidia mtu aliyingia katika janga hili”
alisema Divai na kuongeza:
“Mapitio ya
haraka yanatakiwa katika sheria na sera za dawa za kulevya ili ziweze kusaidia
waathirika wa janga hili; si hapa nchini tuu bali pia kwa ushirikiano na nchi
zingine kwani biashara hii imeenea Duniani kote na inafanyika kimtandao
uliosambaa kote” alitanabaisha.
Naye, Abdalla
Issa maarufu kama Mwakinyo(46), mkazi wa Tanga na kijana anayepata nafuu ya
matumizi ya dawa za kulevya katika nyumba ya kupata nafuu katika Manispaa ya
mji huo; ambaye naye alisema tatizo la sera na sheria kutokuwa za kusaidia
watumiaji, tatizo limekuwa kubwa sana hapa nchini.
Hata hivyo
alisema kuwa matatizo yanajitokeza pale, mtumiaji anapohitaji huduma katika
jamii na badala ya kupewa huonekana kama mhalifu, hivyo kukamatwa au pengine
kushambuliwa na kupigwa kwa kusingiziwa kuwa mwizi.
“Mimi najua yote
haya ni udhaifu wa sera na sheria za udhibiti wa dawa za kulevya ndiyo maana
tunashambuliwa na kupigwa kwa kuonekana kuwa ni wahalifu na siyo janga kama
majanga mengine ambayo yanaweza kumkumba yeyote yule” alisema Issa.
Alisema kuwa
tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya ni tatizo kama matatizo mengine katika
jamii; hivyo ninaiomba jamii kuwaona kuwa wana shida kama walivyo walevi
wengine na siyo wagonjwa wa magonjwa ya akili kwani kuna sera na sheria
zinazowalinda japo hazijakaa vizuri.
Kwa upande wake
mwanasheria wa tume ya kudhibiti dawa za kulevya nchini, Charles Mulamula,
alipoulizwa kuhusu jambo hili alisema kweli sheria na sera bado zina urasimu na
hivyo zinahitaji mapitio ya haraka na kusema kuwa wameshapitia baadhi ya vifungu
bila kutoa ufafanuzi zaidi na kutoa ushauri namna gani viwe ili kusaidia
mapambano ya kutokomeza kemikali hizo.
Alisema kutokana
na madhaifu hayo, yanafainya tume ya kudhibiti dawa hizo kukosa meno; hivyo
inabakia na kazi ya kuratibu tu shughuli za udhibiti na siyo kuweza kuchukua
hatua baada ya kukamata wahusika wa biashara hiyo haramu.
Aidha kwa mujibu
wa sera ya afya ya mwaka 1990 inatoa mwanya kwa watumiaji wa dawa za kulevya
wanapozidiwa na utegemezi kupelekwa katika vitengo vya wagonjwa wa akili katika
hospitali na vituo vya afya; badala ya kuwa na vitengo vyao maalumu vya ushauri
na kupata nafuu na kuacha kabisa.
Hata hivyo
ukipitia kipengere cha 5.4.7 c, katika tamko la sera hiyo ya afya kinasema
serikali kwa kushirikiana na wadau itaimarisha mfumo wa huduma za kinga, tiba
na utengamao wa matumizi ya dawa za kulevya na athari zake.
Aidha, dawa za
kulevya haina sera yake bali inatumia sera ya ukimwi ambayo inasema mashirika
ya serikali yanayoshughulikia matumizi mabaya ya dawa za kulevya kwa
kushirikiana na tume ya kudhibiti ukimwi(TACAIDS), mashirika yasiyokuwa ya
kiserikali(NGO’s) na vikundi vya dini vitaimarisha shughuli zao za kinga na
kutekeleza huduma zinazolengwa za taarifa, elimu na mawasiliano pamoja na
ushauri kwa watumiaji dawa za kulevya.
Kama sera
inasema hivyo, mashirika mangapi ya serikali yameanzishwa na kutimiza majukumu
hayo katika halmashauri zetu; halikadhali mashirika yasiyokuwa ya kiserikali
yapo mangapi ambayo yanafanya kazi hizo kwa moyo kabisa.
No comments:
Post a Comment