Saturday, December 13, 2014

Udhibiti dawa za kulevya mipakani wadorora

·       *  Njia za panya lukuki 
·        * Bodaboda zatumika kuvusha dawa
·       *  Kamanda Nzowa alia na ufinyu wa bajeti  

UDHIBITI wa upitishwaji wa dawa za kulevya katika mipaka na fukwe hapa nchini bado ni tatizo kubwa kutokana na urefu wa fukwe za Bahari ya Hindi na mipaka haswa upande wa Kaskazini ya Tanzania mkoani Kilimanjaro na hivyo kufanya shughuli ya udhibiti kuwa nzito.

Aidha, fukwe peke yake ya Bahari ya Hindi ni takribani kilometa 1,424, ukanda wa Pwani ambapo kwa Mkoa wa Tanga peke yake, kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakembe, kuna takribani Bandari zisizo rasmi 49 ambazo zinauwezekano wa kupitisha bidhaa za magendo pamoja na dawa za kulevya bila kukamatwa.

Tanzania ni nchi pekee iliyojaaliwa kuzungukwa na maziwa kwa upande wa Kaskazini na Magharibi; ambapo Kusini kuna Mto Ruvuma ambao unaitenga na nchi ya Msumbiji hivyo pia upande huo unaweza ukawa njia ya kupitisha bidhaa za magendo, wahamiaji haramu na dawa za kulevya.
Kwanini mashaka hayo?

Amiri Idd (32) ni mkazi wa Kijiji cha Kipumbwi katika Wilaya ya Pangani mkoani Tanga ambapo kuna bandari isiyo rasmi, lakini kwa mujibu wa serikali ya Mkoa hivi sasa inatambulika kwa kusafirisha watu kati ya kijiji hicho na Bandari ya Mkokotoni iliyoko Zanzibar.

Anasema pamoja na serikali kuirasimisha, lakini vitendo vya upitishaji dawa za kulevya unaendelea na yeye mwenyewe kwa muda wa miaka sita alikuwa anafanya biashara haramu ya kuuza Bangi kwenye eneo la Pwani.

Anasema kuwa bangi inapitishwa kwa wingi kwenda na kutoka Zanzibar kupitia fukwe hiyo kutokana na kukosekana kwa mashine maalumu ya kubaini mtu aliyebeba dawa za kulevya, hivyo watu wengi wanapita na mafurushi pamoja na mabegi bila kujulikana wana vitu gani.

“Hapa nyakati za usiku ndiyo safari inaanza kwenda na kutoka Zanzibar na ndipo majahazi kutoka huko yanapofika hapa na mizigo mingi tu. Hakuna udhibiti wala utaratibu wa kukagua kila mzigo, hivyo kama mtu kabeba dawa za kulevya si rahisi kubainika,” anasema kijana huyo.

“Ushahidi mkubwa ni mimi mwenyewe nimefanya biashara ya dawa za kulevya hapa aina ya Bangi kwa takribani miaka sita bila kukamatwa, kitendo hicho tu kinaonyesha kuwa udhibiti hakuna kabisa,” anaongeza Idd.

Safari ya uchunguzi iliendelea katika Wilaya ya Mkinga, katika Kijiji cha Jasini ambako kuna Bandari isiyo rasmi yenye jina hilo la Jasini lakini pia ni kivuko cha miguu kwenda nchi ya jirani ya Kenya katika kijiji cha Vanga.

Ibrahimu Abdallah (50), ambaye ni mkazi wa kijiji cha Jasini na msimamizi na mkatishaji wa ushuru katika mpaka wa nchi ya Kenya na Tanzania katika kijiji cha Vanga anasema pamoja na kazi yake ya kukusanya ushuru mahali hapo, udhibiti wa dawa za kulevya bado hauridhishi.

Anasema kuwa amekuwa akishuhudia watu wakipita na bidhaa za Kenya wakizitoa huko Vanga na kuziingiza Jasini, Tanzania bila kukatwa ushuru wala kuulizwa kama ni bidhaa za biashara au matumizi binafsi.

“Hapa hakuna udhibiti wowote haswa katika bandari zisizo rasmi na vivuko kama hivi katika mipaka yetu hapa nchini, si kwa serikali ya Kenya wala Tanzania hakuna anayelitazama jambo hilo kwa umakini,” anasema kwa uchungu Abdallah na kuongeza: \

“Hapa watu wanapita tu na mizigo yao hakuna hata chombo au mashine ya kuwakagua haswa kwa vitu ambavyo haviwezi kuonekana vizuri kwa macho ambavyo mtu anaweza akawa amevimeza ili kupoteza ushahidi.”

Aidha, Swalehe Alfani (35), ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda anasema ameshuhudia kupitishwa kwa bidhaa kama mifuko ya plastiki pamoja na shehena za mirungi kutoka nchini Kenya ambako wao matumizi ya mirungi siyo kosa kisheria tofauti na hapa nchini.

“Huwa nashuhudia mara nyingi Mirungi na mifuko ya plastiki ikiingizwa kupitia bandari hii isiyo rasmi, wakikwepa kupitia Horohoro maana watakaguliwa na kubainika,” anasema Alfani na kuongeza kuwa: “Hiyo mirungi na mifuko ya plastiki nimeweza kuiona kwa macho lakini hizo dawa nyingine za kulevya kuna uwezekano mkubwa zinapita kwa kuwa wanaopitisha wanaficha vizuri na pengine wanakuwa wamemeza.”

Hata hivyo, anaishauri serikali kuanzisha mpango wa kudhibiti njia hizo mipakani ili kupiga vita biashara haramu ya dawa za kulevya nchini ukizingatia kuwa vijana wengi wanaendelea kuathirika na hata kupoteza maisha kutokana na matumizi yake.

Serikali inathibitisha,

Mwezi Agosti mwaka huu, Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, alisikika katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini akikemea wafanyakazi wa mamlaka ya Bandari (TPA), mamlaka ya mapato (TRA) na Jeshi la polisi kutokana na kuhusika na mtandao wa magendo.

Aliyasema hayo kutokana na kwamba Tanga peke yake ina bandari zisizo rasmi 49, hivyo kuwepo upitishaji wa dawa za kulevya, wahamiaji haramu na biashara ya magendo na pembe za ndovu kwa kiwangi kikubwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya hapa nchini, Kamanda Alfred Nzowa, tatizo la udhibiti lipo kutoka na sababu za ukubwa na upana wa fukwe zetu lakini pia katika Mkoa wa Kilimanjaro pekee kuna njia za vivuko zisizo rasmi 300 mpaka 400 katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ambayo iko mpakani na Kenya.

Anasema kuwa kuwepo na njia za kuvuka zisizo rasmi kwa wingi kiasi hicho ni changamoto kubwa, lakini hawajakata tamaa na kwamba wanaendelea kukabiliana na wahalifu na wanaobainika, sheria inachukuwa mkondo wake.

“Mkoa wa Kilimanjaro peke yake una takribani njia za magendo 300 mpaka 400, hii ni moja ya kikwazo katika udhibiti wa uingizwaji wa dawa za kulevya, lakini bado tunapambana na wahalifu hao,” anasema kamanda Nzowa na kuongeza: “Ukizingatia na ufinyu wa bajeti tunayoipata kutoka serikalini ya bilioni sita (6) kwa mwaka, kazi ya udhibiti wa biashara hii haramu inakuwa na changamoto kubwa sana,” anasema.

Bodaboda zinavyosafirisha Mirungi,

Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya pikipiki zikivusha mirungi kutoka Taveta nchini Kenya na kuziingiza  Moshi mjini kwa mwendo kasi ambao kwa mtu wa kawaida huwezi kuvumilia kupakiwa katika vyombo hivyo vya moto.

“Unashangaa mwendo huo wa pikipiki hizo? Hao ni vijana wa hapahapa Moshi ambao wamesaini kabisa kuwa bora wafe wao lakini mzigo ufike unakokwenda. Hivyo, hapo wameshachukuwa fedha ya kusafirisha mirungi tayari,” anasema kijana mmoja kwa sharti la kutoandikwa jina lake.

Anasema biashara ya mirungi inafanywa kwa wingi katika kivuko hicho cha Holili kwani kipo karibu na mji wa Taveta ulio mpakani kwa upande wa Kenya na kwamba ikifikishwa Moshi na Arusha inasambazwa mikoa mingine kwa magari ya mizigo au abiria.

Anasema kuwa kwa mwenendo huo, udhibiti unakuwa mgumu kwani askari huwa wanashindwa kuwafukuza kwa pikipiki maana huwa katika mwendo kasi na wanakuwa wengi kwa mara moja.

Anaendelea kusema tatizo jingine pia kuna mirungi inayolimwa ndani ya nchi kama wilayani Lushoto, Tanga, Morogoro katika miinuko ya Mgeta na sehemu zinginezo, Arumeru mkoani Arusha hivyo kufanya udhibiti kuwa mgumu sana ukizingatia ukosefu wa vifaa vya kutosha na askari wenye mafunzo maalumu ya udhibiti wa dawa za kulevya.

Wito wake ni kwa taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kuungana kwa pamoja kudhibiti uingizwaji au uzalishwaji wa dawa za kulevya hapa nchini kwa kuwa kukaa kimya ni sawa na kuua nguvu kazi ya Taifa ambao ni vijana.

Safari ya mwandishi wa makala haya iliendelea mpaka kufika katika Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro ambako ndiko mpaka mwingine na nchi ya Kenya uliko ambako kuna vivuko vya Tarakea na Rongai.

Huko mwandishi alishuhudia kushamili kwa biashara za mipakani za halali na magendo, lakini katika wilaya hiyo kuna njia zisizo rasmi zaidi ya 400, na kila mwaka vijana wanaomaliza shule ya msingi wanaingia katika biashara hizo.


Kwa ujumla, maeneo yote hayo hata ukiangalia kwa macho udhibiti wake bado ni dhaifu sana kwani ni eneo pana na kila kilometa ya mraba wanaishi watu zaidi ya 400, hivyo kufanya udhibiti wa kila sehemu ya njia ya panya kuwa ngumu.

No comments:

Post a Comment