Wednesday, December 24, 2014

Methadone inaondoa hamu ya dawa za kulevya,

TIBA ya Methadone inaondoa kabisa hamu ya kutumia dawa za kulevya , hivyo kumfanya mtegemezi wa dawa hizo kuacha kabisa kutegemea na matumizi ya dawa hizo.

Hayo yalisemwa na kijana wa umri wa miaka 30, mkazi wa Mbagala na ambaye hakutaka kutajwa jina lake litajwe katika blogu na ambaye yuko katika mwendelezo wa tiba hiyo katika Hospitali ya Temeke, jijini Dar Es Salaam.

Alisema kuwa, tofauti na kuwekwa katika nyumba ya kupata nafuu ili upunguze hamu kwa masaa 72 bila tiba yeyote na uache kabisa baada ya masaa hayo, Methadone imekuwa ikiondoa hamu pamoja na maumivu ambayo mtumiaji huyapata anapoacha ghafla matumizi ya dawa hizo.

Alisema yeye kwa takribani mwezi wa tatu sasa toka ameanza tiba hiyo; ameacha kabisa matumizi ya dawa za kulevya na sasa yuko katika kituo cha Medecine De Monde (MDM), kilichopo Temeke jijini humo, kwa ajili ya uangalizi na kupata elimu mbalimbali za kuweza kujitegemea baada ya kuacha dawa za kulevya.

Naye kijana mwingine kutoka katika Mkoa wa Tanga mwenye umri wa takribani miaka 38, ambaye naye hakuwa radhi jina lake kuandikwa humu na ambaye yuko katika nyumba ya kupata nafuu iliyoko Mtaa wa Duga, Mkoani humo; alisema nyumba ya kupata nafuu ndiyo suluhisho la kuacha dawa za kulevya kuliko kutumia Methadone.

Alisema kuwa, Methadone nayo iko katika kundi la dawa za kulevya na ni dawa za kulevya na haiwezi kumfanya mtegemezi wa dawa hizo kuacha zaidi ni kumwongezea zaidi utegemezi wa matumizi zaidi.

“Methadone ninavyojua mimi ni dawa ya kulevya tuu, sasa itakuwaje ziweze kukutoa katika utegemezi wa dawa za kulevya? Pamoja na maumivu ya dawa hizoo? Alisema na kuuliza kijana huyo.

Alisema kuwa pia zinagharimu pesa nyingi kuweza kuwapatia waathiriwa wa dawa za kulevya kama vile wanakuwa bado wako katika utegemezi wa dawa zingine za kulevya na kuishauri serikali kuangalia zaidi nyumba za kupata nafuu zaidi kuliko Methadone.

Kwa upande wake, Daktari. Cassian Nyandindi, anayeshughulikia kituo cha Methadone katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar Es Salaam, anasema tiba ya methadone ni mahsusi kwa wategemezi wa dawa za kulevya Duniani kote.

Alisema kuwa imepitishwa na kupasishwa kimataifa kusaidia wategemezi wa dawa za kulevya Ulimwenguni kote na siyo Tanzania peke yake, hivyo anawashauri watu wenye shida ya utegemezi wa dawa za kulevya kuweza kujitokeza katika vituo vya tiba hiyo jijini humo.

Alisema vituo vya tiba hiyo jijini hapo vipo vitatu kwasasa; ambavyo ni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mwananyamala na Temeke; na kuongeza kuwa tiba inagharamiwa na serikali tofauti na nyumba za kupata nafuu ambapo mzazi au ndugu wa mwathirika wa dawa za kulevya wanatakiwa kulipa gharama za kituo husika.

“Ningependa kuchukua fursa kuujulisha umma kuwa tiba ya Methadone kwasasa inapatikana katika vituo vitatu katika Mkoa wa Dar Es Salaamu; ambavyo ni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mwananyamala na Temeke” alisema Dkt. Nyandindi.

Katika uchunguzi wake blogu hii katika Mikoa ya Tanga na Dar Es Salaam katika kupita katika nyumba za kupata nafuu na vituo vya Methadone; ambapo uchunguzi ulibaini katika Mkoa wa Tanga vijana 108,  waliweza kupita katika nyumba ya kupata nafuu.

Aidha, wanane kati yao walipata nafuu kabisa na kurudi katika maisha ya kawaida, 50 kati yao taarifa zao hazikujulikana baada ya kutoka katika nyumba ya kupata nafuu, na 50 waliobakia walirejea katika matumizi ya dawa za kulevya kama mwanzo.


Hata hivyo, katika kituo cha Methadone katika Hospitali ya Temeke, Dar Es Salaam kuna walengwa walioanza kupata tiba ya Methadone 136, walioshindwa kuendelea na tiba hiyo ni tisa, mwanamke mmoja na wanaume wanane na 127 bado wapo na wanaendelea na matibabu vizuri.

No comments:

Post a Comment