Saturday, December 27, 2014

TUTUNZE MAZINGIRA KATIKA MACHIMBO YA KOKOTO


Hapa ni machimbo ya kokoto yaliyopo Mitengo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani

Wednesday, December 24, 2014

Methadone inaondoa hamu ya dawa za kulevya,

TIBA ya Methadone inaondoa kabisa hamu ya kutumia dawa za kulevya , hivyo kumfanya mtegemezi wa dawa hizo kuacha kabisa kutegemea na matumizi ya dawa hizo.

Hayo yalisemwa na kijana wa umri wa miaka 30, mkazi wa Mbagala na ambaye hakutaka kutajwa jina lake litajwe katika blogu na ambaye yuko katika mwendelezo wa tiba hiyo katika Hospitali ya Temeke, jijini Dar Es Salaam.

Alisema kuwa, tofauti na kuwekwa katika nyumba ya kupata nafuu ili upunguze hamu kwa masaa 72 bila tiba yeyote na uache kabisa baada ya masaa hayo, Methadone imekuwa ikiondoa hamu pamoja na maumivu ambayo mtumiaji huyapata anapoacha ghafla matumizi ya dawa hizo.

Alisema yeye kwa takribani mwezi wa tatu sasa toka ameanza tiba hiyo; ameacha kabisa matumizi ya dawa za kulevya na sasa yuko katika kituo cha Medecine De Monde (MDM), kilichopo Temeke jijini humo, kwa ajili ya uangalizi na kupata elimu mbalimbali za kuweza kujitegemea baada ya kuacha dawa za kulevya.

Naye kijana mwingine kutoka katika Mkoa wa Tanga mwenye umri wa takribani miaka 38, ambaye naye hakuwa radhi jina lake kuandikwa humu na ambaye yuko katika nyumba ya kupata nafuu iliyoko Mtaa wa Duga, Mkoani humo; alisema nyumba ya kupata nafuu ndiyo suluhisho la kuacha dawa za kulevya kuliko kutumia Methadone.

Alisema kuwa, Methadone nayo iko katika kundi la dawa za kulevya na ni dawa za kulevya na haiwezi kumfanya mtegemezi wa dawa hizo kuacha zaidi ni kumwongezea zaidi utegemezi wa matumizi zaidi.

“Methadone ninavyojua mimi ni dawa ya kulevya tuu, sasa itakuwaje ziweze kukutoa katika utegemezi wa dawa za kulevya? Pamoja na maumivu ya dawa hizoo? Alisema na kuuliza kijana huyo.

Alisema kuwa pia zinagharimu pesa nyingi kuweza kuwapatia waathiriwa wa dawa za kulevya kama vile wanakuwa bado wako katika utegemezi wa dawa zingine za kulevya na kuishauri serikali kuangalia zaidi nyumba za kupata nafuu zaidi kuliko Methadone.

Kwa upande wake, Daktari. Cassian Nyandindi, anayeshughulikia kituo cha Methadone katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar Es Salaam, anasema tiba ya methadone ni mahsusi kwa wategemezi wa dawa za kulevya Duniani kote.

Alisema kuwa imepitishwa na kupasishwa kimataifa kusaidia wategemezi wa dawa za kulevya Ulimwenguni kote na siyo Tanzania peke yake, hivyo anawashauri watu wenye shida ya utegemezi wa dawa za kulevya kuweza kujitokeza katika vituo vya tiba hiyo jijini humo.

Alisema vituo vya tiba hiyo jijini hapo vipo vitatu kwasasa; ambavyo ni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mwananyamala na Temeke; na kuongeza kuwa tiba inagharamiwa na serikali tofauti na nyumba za kupata nafuu ambapo mzazi au ndugu wa mwathirika wa dawa za kulevya wanatakiwa kulipa gharama za kituo husika.

“Ningependa kuchukua fursa kuujulisha umma kuwa tiba ya Methadone kwasasa inapatikana katika vituo vitatu katika Mkoa wa Dar Es Salaamu; ambavyo ni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mwananyamala na Temeke” alisema Dkt. Nyandindi.

Katika uchunguzi wake blogu hii katika Mikoa ya Tanga na Dar Es Salaam katika kupita katika nyumba za kupata nafuu na vituo vya Methadone; ambapo uchunguzi ulibaini katika Mkoa wa Tanga vijana 108,  waliweza kupita katika nyumba ya kupata nafuu.

Aidha, wanane kati yao walipata nafuu kabisa na kurudi katika maisha ya kawaida, 50 kati yao taarifa zao hazikujulikana baada ya kutoka katika nyumba ya kupata nafuu, na 50 waliobakia walirejea katika matumizi ya dawa za kulevya kama mwanzo.


Hata hivyo, katika kituo cha Methadone katika Hospitali ya Temeke, Dar Es Salaam kuna walengwa walioanza kupata tiba ya Methadone 136, walioshindwa kuendelea na tiba hiyo ni tisa, mwanamke mmoja na wanaume wanane na 127 bado wapo na wanaendelea na matibabu vizuri.

Friday, December 19, 2014

Sheria na Sera za dawa za kulevya hazipo kuwasaidia watumiaji dawa za kulevya,

SHERIA na sera za dawa za kulevya bado hazijasaidia vita ya kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya Duniani kote; hivyo watungaji hawanabudi kuzipitia upya ili zisadie wanaokumbwa na janga la matumizi ya dawa za kulevya
.
Hayo yalisemwa na mwezeshaji na mwelimishaji wa vijana walioathiriwa na dawa za kulevya, Damali Lucas, kutoka taasisi ya Medecine Du Monde (MDM), kituo kinachojishughulisha na kuwasaidia vijana walioamua kuacha matumizi ofisini kwake  jijini Dar Es Salaam.

Alisema, sheria na sera zilizoko zinamwathiri mtumiaji na siyo muingizaji na msambazaji; kwa kuwa mara zote mtumiaji kwa jinsi kemikali hizo zinavyomfanya mwonekano wake wa nje wa kutokujipenda kwa kuwa mchafu kila wakati, hivyo mara zote anaonekana kuwa ni mhalifu.

Alisema kwa kiasi kikubwa wamepata kesi za waathiriwa wa kemikali hizo haramu wamefikishwa kituoni hapo wakiwa wamepigwa na kuumizwa vibaya na wananchi kwa kuonekana kuwa ni wahuni na wahalifu; na pengine walipotaka kupata huduma katika hospitali au vituo vya afya wameshindwa kupata haki zao za msingi kutokana na hali zao na jamii kutokujua sheria inayowalinda.

Aidha, alisema kuwa watunga sera wanatakiwa kuja na sera na sheria zinawasaidia kuliko kuwaona kama wahalifu tu, wakati kuna kundi jingine ambalo linahusika na uingizaji sheria haifanyi lolote kuwatia hatiani.

Hayo pia yalithibitishwa na kijana, Mbwana Divai, Mkazi wa Dar Es Salaam, mtumiaji aliyeacha na kuwa mwelimishaji wa vijana wenzake wanaotaka kuacha matumizi ya kemikali haramu hizo; alisema kuwa kutokuwa na sera na sheria madhubuti kumechangia kwa sehemu kubwa waathiriwa kukosa haki zao za msingi kama kusikilizwa wanapougua na kwenda Hospitali; pamoja na kuwa wako katika matumizi ya dawa hizo haramu.

Divai, alisema yeye alianza kwa kuvuta sigara kwa muda na kuingia katika matumizi ya bangi kutokana na makundi aliyokuwa nayo baada ya kufiwa na wazazi wake wote wawili; ambapo alijikuta akijiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya, hivyo kusema kuwa:

“Tumeshapata matatizo katika jamii ya kutokuaminika hata kama unawaambia kuwa sasa umeacha kutumia kemikali hizo, lakini bado imani inakuwa ndogo; ila kubwa zaidi sheria na sera bado haziko vizuri kuweza kumsaidia mtu aliyingia katika janga hili” alisema Divai na kuongeza:

“Mapitio ya haraka yanatakiwa katika sheria na sera za dawa za kulevya ili ziweze kusaidia waathirika wa janga hili; si hapa nchini tuu bali pia kwa ushirikiano na nchi zingine kwani biashara hii imeenea Duniani kote na inafanyika kimtandao uliosambaa kote” alitanabaisha.

Naye, Abdalla Issa maarufu kama Mwakinyo(46), mkazi wa Tanga na kijana anayepata nafuu ya matumizi ya dawa za kulevya katika nyumba ya kupata nafuu katika Manispaa ya mji huo; ambaye naye alisema tatizo la sera na sheria kutokuwa za kusaidia watumiaji, tatizo limekuwa kubwa sana hapa nchini.

Hata hivyo alisema kuwa matatizo yanajitokeza pale, mtumiaji anapohitaji huduma katika jamii na badala ya kupewa huonekana kama mhalifu, hivyo kukamatwa au pengine kushambuliwa na kupigwa kwa kusingiziwa kuwa mwizi.

“Mimi najua yote haya ni udhaifu wa sera na sheria za udhibiti wa dawa za kulevya ndiyo maana tunashambuliwa na kupigwa kwa kuonekana kuwa ni wahalifu na siyo janga kama majanga mengine ambayo yanaweza kumkumba yeyote yule” alisema Issa.

Alisema kuwa tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya ni tatizo kama matatizo mengine katika jamii; hivyo ninaiomba jamii kuwaona kuwa wana shida kama walivyo walevi wengine na siyo wagonjwa wa magonjwa ya akili kwani kuna sera na sheria zinazowalinda japo hazijakaa vizuri.

Kwa upande wake mwanasheria wa tume ya kudhibiti dawa za kulevya nchini, Charles Mulamula, alipoulizwa kuhusu jambo hili alisema kweli sheria na sera bado zina urasimu na hivyo zinahitaji mapitio ya haraka na kusema kuwa wameshapitia baadhi ya vifungu bila kutoa ufafanuzi zaidi na kutoa ushauri namna gani viwe ili kusaidia mapambano ya kutokomeza kemikali hizo.

Alisema kutokana na madhaifu hayo, yanafainya tume ya kudhibiti dawa hizo kukosa meno; hivyo inabakia na kazi ya kuratibu tu shughuli za udhibiti na siyo kuweza kuchukua hatua baada ya kukamata wahusika wa biashara hiyo haramu.

Aidha kwa mujibu wa sera ya afya ya mwaka 1990 inatoa mwanya kwa watumiaji wa dawa za kulevya wanapozidiwa na utegemezi kupelekwa katika vitengo vya wagonjwa wa akili katika hospitali na vituo vya afya; badala ya kuwa na vitengo vyao maalumu vya ushauri na kupata nafuu na kuacha kabisa.

Hata hivyo ukipitia kipengere cha 5.4.7 c, katika tamko la sera hiyo ya afya kinasema serikali kwa kushirikiana na wadau itaimarisha mfumo wa huduma za kinga, tiba na utengamao wa matumizi ya dawa za kulevya na athari zake.

Aidha, dawa za kulevya haina sera yake bali inatumia sera ya ukimwi ambayo inasema mashirika ya serikali yanayoshughulikia matumizi mabaya ya dawa za kulevya kwa kushirikiana na tume ya kudhibiti ukimwi(TACAIDS), mashirika yasiyokuwa ya kiserikali(NGO’s) na vikundi vya dini vitaimarisha shughuli zao za kinga na kutekeleza huduma zinazolengwa za taarifa, elimu na mawasiliano pamoja na ushauri kwa watumiaji dawa za kulevya.


Kama sera inasema hivyo, mashirika mangapi ya serikali yameanzishwa na kutimiza majukumu hayo katika halmashauri zetu; halikadhali mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yapo mangapi ambayo yanafanya kazi hizo kwa moyo kabisa. 

Saturday, December 13, 2014

Udhibiti dawa za kulevya mipakani wadorora

·       *  Njia za panya lukuki 
·        * Bodaboda zatumika kuvusha dawa
·       *  Kamanda Nzowa alia na ufinyu wa bajeti  

UDHIBITI wa upitishwaji wa dawa za kulevya katika mipaka na fukwe hapa nchini bado ni tatizo kubwa kutokana na urefu wa fukwe za Bahari ya Hindi na mipaka haswa upande wa Kaskazini ya Tanzania mkoani Kilimanjaro na hivyo kufanya shughuli ya udhibiti kuwa nzito.

Aidha, fukwe peke yake ya Bahari ya Hindi ni takribani kilometa 1,424, ukanda wa Pwani ambapo kwa Mkoa wa Tanga peke yake, kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakembe, kuna takribani Bandari zisizo rasmi 49 ambazo zinauwezekano wa kupitisha bidhaa za magendo pamoja na dawa za kulevya bila kukamatwa.

Tanzania ni nchi pekee iliyojaaliwa kuzungukwa na maziwa kwa upande wa Kaskazini na Magharibi; ambapo Kusini kuna Mto Ruvuma ambao unaitenga na nchi ya Msumbiji hivyo pia upande huo unaweza ukawa njia ya kupitisha bidhaa za magendo, wahamiaji haramu na dawa za kulevya.
Kwanini mashaka hayo?

Amiri Idd (32) ni mkazi wa Kijiji cha Kipumbwi katika Wilaya ya Pangani mkoani Tanga ambapo kuna bandari isiyo rasmi, lakini kwa mujibu wa serikali ya Mkoa hivi sasa inatambulika kwa kusafirisha watu kati ya kijiji hicho na Bandari ya Mkokotoni iliyoko Zanzibar.

Anasema pamoja na serikali kuirasimisha, lakini vitendo vya upitishaji dawa za kulevya unaendelea na yeye mwenyewe kwa muda wa miaka sita alikuwa anafanya biashara haramu ya kuuza Bangi kwenye eneo la Pwani.

Anasema kuwa bangi inapitishwa kwa wingi kwenda na kutoka Zanzibar kupitia fukwe hiyo kutokana na kukosekana kwa mashine maalumu ya kubaini mtu aliyebeba dawa za kulevya, hivyo watu wengi wanapita na mafurushi pamoja na mabegi bila kujulikana wana vitu gani.

“Hapa nyakati za usiku ndiyo safari inaanza kwenda na kutoka Zanzibar na ndipo majahazi kutoka huko yanapofika hapa na mizigo mingi tu. Hakuna udhibiti wala utaratibu wa kukagua kila mzigo, hivyo kama mtu kabeba dawa za kulevya si rahisi kubainika,” anasema kijana huyo.

“Ushahidi mkubwa ni mimi mwenyewe nimefanya biashara ya dawa za kulevya hapa aina ya Bangi kwa takribani miaka sita bila kukamatwa, kitendo hicho tu kinaonyesha kuwa udhibiti hakuna kabisa,” anaongeza Idd.

Safari ya uchunguzi iliendelea katika Wilaya ya Mkinga, katika Kijiji cha Jasini ambako kuna Bandari isiyo rasmi yenye jina hilo la Jasini lakini pia ni kivuko cha miguu kwenda nchi ya jirani ya Kenya katika kijiji cha Vanga.

Ibrahimu Abdallah (50), ambaye ni mkazi wa kijiji cha Jasini na msimamizi na mkatishaji wa ushuru katika mpaka wa nchi ya Kenya na Tanzania katika kijiji cha Vanga anasema pamoja na kazi yake ya kukusanya ushuru mahali hapo, udhibiti wa dawa za kulevya bado hauridhishi.

Anasema kuwa amekuwa akishuhudia watu wakipita na bidhaa za Kenya wakizitoa huko Vanga na kuziingiza Jasini, Tanzania bila kukatwa ushuru wala kuulizwa kama ni bidhaa za biashara au matumizi binafsi.

“Hapa hakuna udhibiti wowote haswa katika bandari zisizo rasmi na vivuko kama hivi katika mipaka yetu hapa nchini, si kwa serikali ya Kenya wala Tanzania hakuna anayelitazama jambo hilo kwa umakini,” anasema kwa uchungu Abdallah na kuongeza: \

“Hapa watu wanapita tu na mizigo yao hakuna hata chombo au mashine ya kuwakagua haswa kwa vitu ambavyo haviwezi kuonekana vizuri kwa macho ambavyo mtu anaweza akawa amevimeza ili kupoteza ushahidi.”

Aidha, Swalehe Alfani (35), ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda anasema ameshuhudia kupitishwa kwa bidhaa kama mifuko ya plastiki pamoja na shehena za mirungi kutoka nchini Kenya ambako wao matumizi ya mirungi siyo kosa kisheria tofauti na hapa nchini.

“Huwa nashuhudia mara nyingi Mirungi na mifuko ya plastiki ikiingizwa kupitia bandari hii isiyo rasmi, wakikwepa kupitia Horohoro maana watakaguliwa na kubainika,” anasema Alfani na kuongeza kuwa: “Hiyo mirungi na mifuko ya plastiki nimeweza kuiona kwa macho lakini hizo dawa nyingine za kulevya kuna uwezekano mkubwa zinapita kwa kuwa wanaopitisha wanaficha vizuri na pengine wanakuwa wamemeza.”

Hata hivyo, anaishauri serikali kuanzisha mpango wa kudhibiti njia hizo mipakani ili kupiga vita biashara haramu ya dawa za kulevya nchini ukizingatia kuwa vijana wengi wanaendelea kuathirika na hata kupoteza maisha kutokana na matumizi yake.

Serikali inathibitisha,

Mwezi Agosti mwaka huu, Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, alisikika katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini akikemea wafanyakazi wa mamlaka ya Bandari (TPA), mamlaka ya mapato (TRA) na Jeshi la polisi kutokana na kuhusika na mtandao wa magendo.

Aliyasema hayo kutokana na kwamba Tanga peke yake ina bandari zisizo rasmi 49, hivyo kuwepo upitishaji wa dawa za kulevya, wahamiaji haramu na biashara ya magendo na pembe za ndovu kwa kiwangi kikubwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya hapa nchini, Kamanda Alfred Nzowa, tatizo la udhibiti lipo kutoka na sababu za ukubwa na upana wa fukwe zetu lakini pia katika Mkoa wa Kilimanjaro pekee kuna njia za vivuko zisizo rasmi 300 mpaka 400 katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ambayo iko mpakani na Kenya.

Anasema kuwa kuwepo na njia za kuvuka zisizo rasmi kwa wingi kiasi hicho ni changamoto kubwa, lakini hawajakata tamaa na kwamba wanaendelea kukabiliana na wahalifu na wanaobainika, sheria inachukuwa mkondo wake.

“Mkoa wa Kilimanjaro peke yake una takribani njia za magendo 300 mpaka 400, hii ni moja ya kikwazo katika udhibiti wa uingizwaji wa dawa za kulevya, lakini bado tunapambana na wahalifu hao,” anasema kamanda Nzowa na kuongeza: “Ukizingatia na ufinyu wa bajeti tunayoipata kutoka serikalini ya bilioni sita (6) kwa mwaka, kazi ya udhibiti wa biashara hii haramu inakuwa na changamoto kubwa sana,” anasema.

Bodaboda zinavyosafirisha Mirungi,

Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya pikipiki zikivusha mirungi kutoka Taveta nchini Kenya na kuziingiza  Moshi mjini kwa mwendo kasi ambao kwa mtu wa kawaida huwezi kuvumilia kupakiwa katika vyombo hivyo vya moto.

“Unashangaa mwendo huo wa pikipiki hizo? Hao ni vijana wa hapahapa Moshi ambao wamesaini kabisa kuwa bora wafe wao lakini mzigo ufike unakokwenda. Hivyo, hapo wameshachukuwa fedha ya kusafirisha mirungi tayari,” anasema kijana mmoja kwa sharti la kutoandikwa jina lake.

Anasema biashara ya mirungi inafanywa kwa wingi katika kivuko hicho cha Holili kwani kipo karibu na mji wa Taveta ulio mpakani kwa upande wa Kenya na kwamba ikifikishwa Moshi na Arusha inasambazwa mikoa mingine kwa magari ya mizigo au abiria.

Anasema kuwa kwa mwenendo huo, udhibiti unakuwa mgumu kwani askari huwa wanashindwa kuwafukuza kwa pikipiki maana huwa katika mwendo kasi na wanakuwa wengi kwa mara moja.

Anaendelea kusema tatizo jingine pia kuna mirungi inayolimwa ndani ya nchi kama wilayani Lushoto, Tanga, Morogoro katika miinuko ya Mgeta na sehemu zinginezo, Arumeru mkoani Arusha hivyo kufanya udhibiti kuwa mgumu sana ukizingatia ukosefu wa vifaa vya kutosha na askari wenye mafunzo maalumu ya udhibiti wa dawa za kulevya.

Wito wake ni kwa taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kuungana kwa pamoja kudhibiti uingizwaji au uzalishwaji wa dawa za kulevya hapa nchini kwa kuwa kukaa kimya ni sawa na kuua nguvu kazi ya Taifa ambao ni vijana.

Safari ya mwandishi wa makala haya iliendelea mpaka kufika katika Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro ambako ndiko mpaka mwingine na nchi ya Kenya uliko ambako kuna vivuko vya Tarakea na Rongai.

Huko mwandishi alishuhudia kushamili kwa biashara za mipakani za halali na magendo, lakini katika wilaya hiyo kuna njia zisizo rasmi zaidi ya 400, na kila mwaka vijana wanaomaliza shule ya msingi wanaingia katika biashara hizo.


Kwa ujumla, maeneo yote hayo hata ukiangalia kwa macho udhibiti wake bado ni dhaifu sana kwani ni eneo pana na kila kilometa ya mraba wanaishi watu zaidi ya 400, hivyo kufanya udhibiti wa kila sehemu ya njia ya panya kuwa ngumu.

Friday, March 1, 2013

http://yield2me.com/-100764.htm

GREEN WORLD WAINGIA MTWARA KWA KISHINDO

Watalaam wa Green World wakiwa katika ukumbi wa Lutheran wakitambulisha bidhaa na huduma wanazozitoa kwa waandishi wa habari, hawako pichani

Mwandishi wa habari wa redio Maria Mtwara akitolewa sumu mwilini kwa kifaa maalumu

Mtalaam wa Green World Dina kutoka Dar es salaam akiwa makini kutambulisha bidhaa zao mbele yake mezani

Saturday, December 1, 2012

KUKUA KWA BIASHARA NANGURUKULU

Biashara kama kawaida Nangurukulu, akinamama wauza samaki wakiwauzia wasafairi wa kwenda Mikoa ya Lindi na Mtwara lakini pia wale wa kwenda Dar es salaam.